Mitandao ya Kijamii inavyounda ushiriki wa Vijana Kwenye Uchaguzi
Author: Harold Henry Mafita (Tanzania) | 3rd place winner of the 2024 Youth & Elections in Africa Essay Contest | In Swahili
Utangulizi
Sehemu kubwa ya idadi ya watu katika bara la Africa ni vijana, kundi hili ndilo linaloongoza katika kufikia na kutumia mitandao ya kijamii kwaajili ya mawasiliano, burudani, kufanya biashara na kupata taarifa mbalimbali ikiwemo zile za kisasa. Kipindi cha hivi karibuni mitandao ya kijamii imeibuka kuwa chombo chenye nguvu katika kuunda ufahamu na ushiriki wa vijana kwenye siasa. Majukwaa ya mitandao hii kama Whatsapp, Twitter (X), Facebook na Instagram yanatumiwa kwa kiasi kikubwa kuwafikia wapiga kura vijana, kusambaza uelewa wa kisiasa na kuchochea kampeni fulani fulani za kijamii za kudai haki kwa umoja, mfano vyama vya upinzani Tanzania vinasukuma sana kampeni ya #Katibampya kwa njia za mitandao ya kijamii. Mabadiliko haya yameanzisha njia na mwenendo mpya katika ushiriki wa vijana kwenye michakato ya kisiasa, sasa usambazaji wa taarifa ni haraka mno kuliko hapo nyuma, uwezo wa watu kujua jambo na kuwa na sauti moja ni mkubwa kuliko popote kwenye historia na vivyo hivyo taarifa za kisasa zimewafikia kwa haraka sana vijana na kuongeza hamasa na ushiriki wao kwenye chaguzi bila kujali jinsia zao. Insha hii inalenga kuelezea namna ambavyo maendeleo haya ya kidigitali hususani kwenye mitandao ya kijamii yameongeza ushiriki wa vijana kwenye uchaguzi.
Jinsi Mitandao ya Kijamii inavyounda Ushiriki wa Vijana Katika Uchaguzi; Kuongeza Ufahamu wa Kisiasa
Taarifa zinazohusu muenendo wa kisiasa zimewafikia vijana kwa njia ya simu za mikononi na/au kompyuta pamoja na huduma ya intaneti kwa kutumia mitandao ya kijamii, sasa vijana wanaweza kuelewa na kufahamu vizuri juu ya umuhimu wa kushiriki katika kutengeneza serikali itakayo kuwa msaada kwao, vijana Wana ajenda zao kama ajira, kuwezeshwa kujiajiri, mikopo ya masomo, mambo yahusuyo jinsia nk, vijana wanaweza kuona kwa urahisi kupitia mitandao ya kijamii ilani na sera za chama kipi cha kisiasa zinaendana na ajenda zao, hii inachochea hali ya vijana kuona ni vema wao pia kushiriki kuchagua watu wanaowafaa ili waweze kutimiza matamanio ya maisha yao kama vijana.
Mitandao ya kijamii inajenga sauti ya pamoja kwa vijana kabla ya uchaguzi
Kupitia mitandao ya kijamii vijana wanaweza kujenga vuguvugu juu ya nini wanataka na nani wanaoona anafaa kushika nafasi kwani mitandao hii inauwezo wa kuwakutanisha vijana bila kujali umbali, nguvu hii inatoa hamasa hata kwa kijana asiekuwa na muamko wa kushiriki uchaguzi kuona inatakiwa na yeye pia kushiriki kukubali au kupinga vuguvugu la kisiasa linaloletwa na vijana wenzake, kitu kinachoongeza ushiriki wa vijana kwenye kufanya maamuzi kwa njia ya sanduku la kura.
Mitandao ya kijamii inatumika kufichua kutokuwajibika kisiasa kwa viongozi
Kama nilivoeleza hapo awali kuwa vijana ndio watumiaji wakubwa wa mitandao ya kijamii, ambapo wanaharakati wa kisiasa nao wametumia majukwaa haya ya mitandao hii kuonesha namna ambavyo serikali au mtu wa nafasi fulani hajawajibika kwa manufaa ya vijana au jamii kwa upana wake, taarifa hizi kwa vijana zinakuwa ni kama mafuta ndani ya moto kwani huwapa hasira ya kutaka kuhusika kufanya maamuzi ya kisiasa ya kuunda serikali upya ili kuleta uwajibikaji, kama uchaguzi ni huru basi vijana hupeleka hasira hizo kwenye masanduku ya kura.
Serikali, asasi za kiraia, mashirika ya umma na binafsi yanatumia mitandao ya kijamii kushawishi ushiriki wa vijana kwenye uchaguzi.
Maudhui mbalimbali hupandishwa na vyombo hivi kuhamasisha ushiriki wa vijana katika uchaguzi, vyombo hivi hutumia njia zingine kama redio, televisheni na magazeti lakini linapokuja swala la kuwafikia vijana basi kurasa za mitandao ya kijamii za vyombo hivi hutumika kuwafikia vijana na kuwaelimisha juu ya haki na majukumu yao na kuwapa hamasa ya kujiandikisha, kutokea na kupiga kura kwa usahihi pasipo kuharibu kura zao.
Mitandao ya kijamii inasaidia kuongeza ufuatiliaji wa muenendo wa matokeo ya uchaguzi katika maeneo mengine na kuvutia ushiriki wa vijana.
Uchaguzi hufanyika maeneo mbalimbali, matokeo ya jumla huaathiriwa na matokeo madogomadogo ya maeneo mengine. Vijana wanavutiwa na kutopotea kwa nguvu zao na kutoibiwa kwa uchaguzi, muenendo wa matokeo ya uchaguzi Kwenye mitandao ya kijamii inasaidia kuwaonesha vijana kuwa haki yao iko mikono salama na maamuzi yaliyofanywa na watu wengine kutoka maeneo mengine hayajadharauliwa na kuibiwa, hali ambayo huwavutia kushiriki hata wakati mwingine kwani uchaguzi inakuwa silaha tosha kwao kuwawajibisha viongozi wao.
Serikali na mamlaka za mawasiliano za nchi za kiafrika huaribu mno mtazamo na hamasa ya vijana kwa kushusha au kuzima kabisa kwa makusudi huduma ya intaneti, jambo hili limeshuhudiwa na mamlaka za kusimamia uchaguzi zisizofungamana na vyama vyetu vya kisiasa yaani taasisi za kimataifa, kuwa kasi ya huduma ya intaneti huwa chini sana kipindi cha uchaguzi, jambo linalozua maswali mengi kwa vijana kuhusu kinachoendelea, ikumbukwe vijana hawaingii mtandaoni kufatilia uchaguzi tu bali biashara, burudani, habari nk, kwaio uchaguzi kuhusishwa na kushuka kwa kasi ya huduma ya intaneti inasababisha vijana kuchukia tukio hili na kutotaka kushiriki kwani linaharibu shughuli zao na haliko wazi.
Hitimisho
Maendeleo ya kidigitali katika ulimwengu wa leo ni chanzo cha mabadiliko ya mambo mengi sana, uendeshaji wa taasisi za umma na binafsi, serikali na shughuli mbalimbali umebadilishwa mno. Kizazi cha vijana wa leo kinaishi katika wakati wa kidigitali ambapo kila kitu kinaweza fanyika kiganjani, kuanzia kwenye kujifunza ujuzi mpya mpaka kufuatilia muenendo wa kisiasa katika nchi zao.
Kuunda ushiriki wa vijana katika shughuli nzima za uchaguzi, mitandao ya kijamii kama sehemu ya maendeleo ya kidigitali haina budi kutumiwa ili kuelimisha, kuhamasisha na kuchochea ushiriki wa vijana, ni vema sasa taasisi zenye mamlaka kutia nguvu ili kuwaingiza vijana katika haki hii hadhimu ya kuchagua nani na nani wataunda serikali za mitaa na serikali kuu.
