Jitihada za Kufanikisha Ukuaji wa Matumizi ya Intaneti Tanzania: Elimu na Haki za Mtumiaji

Pollicy
5 min readFeb 8, 2024

--

Takwimu za mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA), zinaonyesha kuwa watumiaji wa intaneti wanaongezeka kwa kasi kubwa sana nchini Tanzania mpaka kufikia watumiaji 34,469,022 kwa mwaka 2023, kutoka watumiaji 23,808,942 kwa mwaka 2018 kukiwa na ongezeko la watumiaji 10,660,080 ndani ya miaka mitano. Licha ya kuwa na ongezeko kubwa la watumiaji wa intaneti kati ya watumiaji hao, ni asilimia ndogo sana wanaojua namna ya kutumia intaneti kwa usahihi na manufaa zaidi.

Matumizi ya intaneti yanaenda sambamba na matumizi ya majukwaa ya kidigitali, na hapa ndipo tofauti kubwa inatokea kimatumizi baina ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii pamoja na majukwaa ya kidigitali. Utofauti huu unatokana na sababu mbalimbali kulingana na Umri, Jinsia, Elimu na tofauti mbali mbali katika jamii

Kwenye jamii zetu za kiafrika, hasa Tanzania, kumekuwa na pengo kubwa katika matumizi ya majukwaa ya kidigitali na intaneti kwa ujumla, yaani kuna baadhi ya makundi katika jamii zetu yanawekwa kando kabisa katika kutumia majukwaa haya ya kidijitali hivyo basi kukosa uelewa wa kutumia majukwaa haya ya kidijitali kwa manufaa yao binafsi na kwa jamii zao.

Wanawake ndio kundi kubwa kabisa kwenye jamii zetu lililopo nyuma katika matumizi ya kidigitali na majukwaa yake kwa ujumla, na hii ni kutokana na sababu mbalimbali — ukosefu wa elimu ya matumizi sahihi ya majukwaa ya kidigitali, kushindwa kumudu gharama za vifaa vya kidigitali na vifurushi vya intaneti, mila na utamaduni, kasumba mbali mbali, na nyingine nyingi hivyo basi ikiwa kuna sababu kama hizi zinazokwamisha matumizi na haki ya msingi kabisa ya mwanamke wa karne ya sasa ya kutumia intaneti na majukwaa ya kidigitali kwa maendeleo binafsi na jamii yao, serikali na washika dau wana kazi kubwa ya kuhakikisha kuwa kundi hili muhimu kwenye jamii yetu linaweza kupata elimu na kujengewa uwezo mzuri wa kutumia majukwaa ya kidijitali kwa manufaa yao na kwa jamii nzima.

Kama kuku akusanyavyo vifaranga vyake na kuvitunza basi katika matumizi ya intaneti na majukwaa ya kidijitali ndani ya Tanzania kuna sheria mbali mbali zinazoongoza watumiaji wa intaneti na majukwaa ya kidjitali ili kulinda watumiaji hao na kuwawajibisha kulingana na sheria iliyowekwa wale wanaokiuka matumizi sahihi ya Intaneti na majukwaa ya kidigitali kwa ujumla kwa kuwa matumizi ya majukwaa haya ya kidigitali yana faragha za watu na hivyo kuwa moja kati ya nyenzo muhimu inayohitajika kulindwa kwa nguvu kubwa sana.

Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi ya mwaka 2022 inakataza kabisa matumizi au ukusanyaji wa data za mtu mwingine kutumika au kusambazwa bila idhini au kibali kutoka mamlaka husika, katika sheria iliyopendekezwa na Bunge la Tanzania, katika kipengele cha tisa ibara ya 60 -1 inasema kuwa “mkusanyaji ambaye bila sababu za msingi atafichua taarifa binafsi kwa njia yoyote ambayo haiendani na madhumuni ambayo taarifa hiyo imekusanywa anatenda kosa”

Ikiwa sheria zipo na zinaweza kuwalinda kikamilifu watumiaji wa majukwaa ya kidigitali, swali kubwa ni kwamba je! watumiaji wa majukwaa hayo ya kidigitali wana uelewa kuhusu sheria zilizopo na ni kwa namna gani zinafanya kazi? Ni kwa kiwango gani zinamlinda mtumiaji wa majukwaa ya kidigitali?

Katika jukwaa la JamiiForums mwaka 2023, mdau mmoja amelalamikia utaratibu wa baadhi ya watumishi wa halmashauri ya Mvomero, Morogoro aliodai wamekuwa wakitoa namba za watumishi kwa taasisi za fedha ili kuwashawishi kuchukua mikopo, anaeleza baada ya kuripoti katika Halmashauri hiyo, alianza kupokea Simu na jumbe zinazohusu mikopo. Alipowauliza namba zake wametoa wapi walimjibu wanapewa na watu wa utumishi.

Je, jamii yetu ya watanzania wanafahamu kwamba, kuuza au kuchakata taarifa binafsi ikiwemo namba ya simu kinyume na madhumuni ya awali ya ukusanyaji wa taarifa hizo ni uvunjifu wa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi ya 2022 na unaweza kumshtaki mkusanyaji? Pia sheria hii inafanya kazi katika mitandao ya kijamii pia kuhakikisha hakuna uuzwaji na usambazaji wa data binafsi za watumiaji wa mitandao ya kijamii na majukwaa ya kidijitali kwa ujumla.

Nini kifanyike ili watumiaji wa intaneti na majukwaa ya kidigitali ndani ya Tanzania na Afrika kwa ujumla waweze kuwa na uelewa wa matumizi sahihi ya majukwaa ya kidigitali pamoja na kujua nia kwa namna gani wanaweza kunufaika nayo na kubwa zaidi kujua haki zao na kwa namna gani wanaweza kuwa salama katika majukwaa ya kidijitali kwani sheria zipo na zipo kwaajili yao.

Kwanza kabisa, serikali na sekta binafsi waweze kutoa elimu juu matumizi sahihi ya majukwaa ya kidjitali ili watumiaji wake waweze kunufaika na majukwaa hayo kwani ni ukweli usiopingika kuwa kwa karne ya sasa watu wanahitaji kutumia intanet kwa manufaa yao ikiwa ni kwa kuingiza kipato, kupata burudani, elimu na sababu nyingine nyingi na hii inatokana na ukuaji mkubwa wa sayansi na teknolojia

Pili, serikali na sekta binafsi waweze kutoa elimu juu ya haki za watumiaji wa intaneti na ni kwa namna gani sheria inawalinda watumiaji hao na inawabana wakiukwaji wa sheria iliyowekwa, ikiwa watumiaji wa intaneti watapewa elimu ya kina kuhusu namna bora ya kutumia intaneti, bila shaka jamii bora itajengwa na yenye kujua namna ya kutumia intaneti kwa manufaa zaidi.

Tatu, rai itolewe juu matumizi sahihi ya majukwaa ya kidijitali kwani siku za karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la kusambaa kwa maudhui na data za faragha bila kuhusishwa kwa wahusika wa data hizo, sheria iko bayana kwani hairuhusu uchakataji wa data binafsi ikiwa anayehitaji kuchakata data hizo hajaidhinishwa na serikali.

Nne, ni muhimu kutafuta usaidizi wa haraka ikiwa kuna kosa limetokea, yaani taarida zako binafsi zimetolewa bila ya wewe muhusika na mtumiaji hujaidhinisha, muhimu kufuata taratibu za kisheria kwa msaada zaidi

Hivyo basi, ongezeko la watumiaji wa intaneti ndani na nje ya Tanzania ni dalili tosha kuwa maendeleo ya sekta ya mawasiliano inakua kwa kasi kubwa sana hivyo watumiaji wa intaneti wawe makini sana na wajue ni sheria gani zinawalinda katika kutumia intaneti na majukwaa ya kidigitali kwa ujumla.

Imeandikwa na Edward Stephen Mbaga.

This blog is authored by Edward Mbaga, the 4th place winner of the Digital Ambassador Program ‘Kalamu za Kidigitali’ Blog Competition, and edited by our dedicated team at Pollicy. Pollicy established the Digital Ambassador Program (DAP) to empower youth with digital resilience skills on safety and security especially women in higher learning institutions. The Digital Ambassador Program is proud to collaborate with The LaunchPad Tanzania, Tanzania AI Lab & Community, Uganda Institute of Information and Communications Technology, Centre for Technology Disputes Resolution, Internet Society Uganda Chapter, and Civil Rights Defenders.

--

--

Pollicy
Pollicy

Written by Pollicy

Re-designing Government for Citizens

No responses yet